;
Hali hiyo inajulikana kama vaccine-induced immune thrombocytopenia and thrombosis (VITT). Ilisababishwa na mabadiliko nadra katika mfumo wa kinga ya mwili. Kwa watu walioathirika, kulikuwa na hitilafu katika vinasaba vya seli za B zinazozalisha kingamwili. Mabadiliko hayo yalisababisha mwili kutengeneza kingamwili zisizo za kawaida. Kingamwili hizo zilishambulia kimakosa protini ya kawaida ya damu iitwayo platelet factor 4 (PF4).
Utafiti ulibaini kuwa protini fulani ndani ya adenovirus iliyotumika kwenye chanjo ilifanana sana na PF4. Kutokana na mfanano huo, mfumo wa kinga ulichanganya protini ya chanjo na ile ya mwili katika mchakato unaojulikana kama molecular mimicry. Kingamwili zilipojishikiza kwenye PF4, ziliamsha pleteleti za damu ambazo husababisha damu kuganda. Hii ilisababisha kutokea kwa vifungo vya damu katika maeneo yasiyo ya kawaida kama ubongo au tumboni. Wakati huo huo, kiwango cha pleteleti za damu kilishuka, hali iliyoongeza hatari ya kutokwa damu kupita kiasi.
Watafiti wamegundua pia kuwa wagonjwa wengi walioathirika walikuwa na muundo unaofanana wa kingamwili, jambo lililothibitisha kuwa tatizo hilo lilikuwa na chanzo kimoja cha kibayolojia. Inaaminika kuwa baadhi yao huenda walikuwa tayari wamewahi kuambukizwa adenovirus hapo awali, hali iliyoufanya mfumo wao wa kinga kuwa tayari kuitikia kwa nguvu zaidi walipopokea chanjo.
Utafiti huo ulithibitisha kuwa VITT ilikuwa nadra mno, ikitokea kwa takribani mtu mmoja kati ya 200,000 waliopokea chanjo ya Oxford-AstraZeneca barani Ulaya na Australia au Johnson & Johnson nchini Marekani. Tatizo hili halikuhusishwa na chanjo za mRNA kama Moderna na Pfizer/BioNTech.
Ugunduzi muhimu zaidi ni kwamba sasa protini mahsusi ya adenovirus iliyosababisha tatizo hilo imetambuliwa. Hii inamaanisha kuwa watengenezaji wa chanjo wanaweza kuibadilisha au kuiondoa ili kuzuia athari hiyo nadra bila kupunguza ufanisi wa chanjo. Matokeo haya yanaweza pia kusaidia kuboresha usalama wa chanjo nyingine zinazotumia adenovirus kwa magonjwa kama Ebola, na hivyo kuimarisha zaidi imani ya umma katika sayansi na chanjo.