;
Waziri wa mazingira Deborah Barasa ameagiza kufungwa mara moja kwa kampuni ya Shreeji Chemicals Limited yenye makao yake eneo la Mlolongo kaunti ya Machakos kwa kukiuka sheria za mamlaka ya usimamizi wa mazingira NEMA
Katika ziara ya ghafla waliofanya kwenye kampuni hiyo jumanne ya tarehe 5 mwezi Mei waziri Barasa aliyeandamana na mkurugenzi mkuu wa NEMA Mamo B. Mamo walizuiliwa kwa muda kuingia kwenye kampuni hiyo na walinzi waliodai kupewa maagizo hayo na usimamizi wa kampuni hiyo
Iliwalazimu maafisa wa polisi kuingilia kati ambapo baada ya kuingia waziri Barasa na kikosi cha maafisa wakuu kutoka wizara ya mazingira na mamlaka ya NEMA walibaini kuwa kampuni hiyo ya Shreeji Chemical Limited imekiuka sheria mbalimbali za mamlaka ya NEMA kisha wakaagiza ifungwe mara moja
Mkurugenzi mkuu wa NEMA Mamo B. Mamo alisema maafisa 3 wakuu wa kampuni hiyo wamekamatwa watawasilishwa mahakani ambapo watashtakiwa kwa makosa mbalimbali likiwemo la kuzuia maafisa wa NEMA kukagua mazingira ya kazi ya kampuni hiyo sawa na kukiuka sheria zengine za NEMA
Wakati wa oparesheni hiyo ya kusaka kampuni zinazoelekeza uchafu kwenye mito eneo hilo la Athiriver waziri Barasa vilevile alitoa makataa ya siku 7 kwa kampuni ya CANON Chemicals Limited kuhakikisha inafuata vikamilifu sheria za mamlaka ya NEMA la sivyo vilevile aagize ifungwe
Barasa anasema oparesheni hii iliandaliwa baada ya kuabinika kuwa baadhi ya kampuni zilikua zimeanza kuelekeza majitaka kwenye vyanzo vya mto Nairobi na mto Athi baada ya ukaguzi wa mara ya mwisho uliokua umehakikisha hakuna kampuni inayoelekeza uchafu kwenye mito
"Nimeagiza mamlaka ya NEMA kukagua kampuni zote ili kuhakikisha hakuna kampuni inayoelekeza majitaka kwenye mito. Oparesheni hii itakayoandaliwa kote nchini itaandaliwa kwa uwazi na haitamsaza yeyote. alisema Barasa
Alisema licha ya kuwa kampuni zaidi ya 100 zilikaguliwa mwaka jana nyingi ya kampuni hizo zimetelekeza matakwa zilizotakiwa kuangazi
Aliorodhesha baadhi ya sababu zinazoweza kuchangia kufungwa kwa kampuni hizo akisema miongoni mwao ni pamoja na kampuni kuhudumu pasi na mikakati nzuri ya kutupa taka, kuelekeza majitaka, kuchoma taka pasi na mikakati hitajika miongoni mwa sababu zengine
Waziri huyo vilevile alikariri haja kwa wamiliki wa majengo kujiepusha na hulka ya kunyakua ardhi na kujenga kwenye mito akisema serikali itaendelea kubomoa majengo yaliyojengwa kandokando ya mito
Hatua hii ya serikali inaonekana kuwa mkakati mpya wa kufufua juhudi za kusafisha mto Nairobi ambao kwa muda umetajwa kuchafuliwa majitaka kutoka kwa kampuni hasa zilizoko eneo hilo la Mlolongo na Athiriver